Monday, October 24, 2011

Waraka wa Kinabo:Kwa Serikali hii,daima tutaomboleza uzembe

Na Edward Kinabo

NIMERUDI tena, kwa uchungu na hisia nzito. Mungu azilaze mahali pema peponi roho za Watanzania wenzetu waliopoteza maisha kwenye maafa ya mv Spice Islanders. Mungu azijaze moyo wa uvumilivu na ujasiri familia zao, ndugu, jamaa na rafiki zao wa karibu, hususan katika kipindi hiki kichungu.

Wapo watakaosema “ajali haina kinga”, na wapo watakaodiriki kusema, “Wamekufa kwa sababu hiyo ndiyo siku yao waliyoandikiwa na Mungu”, kwamba “kazi ya Mungu haina makosa”. Fikra hizi, zinazoonekana kuwa za kiungwana na za kumcha-Mungu, ndizo zinazoifanya Serikali hii ya kizembe kuendelea na uzembe wake na kusababisha wananchi wengi kupoteza maisha katika mazingira ya kizembezembe, uzembe ambao na sisi kwa kujisahau, tumekuwa tukiulinda kwa kuwa na fikra na misemo kibao ya kumsingizia Mungu.

Ni kweli, kazi ya Mungu haina makosa, lakini kazi ya Mungu haipaswi kuingiliwa na mkono wa binadamu. Mungu wetu hawezi kuwa mzembe kama viongozi wa Serikali ya CCM, na ile ya Umoja wa Kitaifa kule Zanzibar. Na hata ikimlazimu kuwachukua watu wake, hana sababu ya kuwachukua kizembezembe.

Najua, wapo waungwana wengine watakaosema kuwa si ustaarabu kuchanganya siasa na suala la ajali iliyopoteza maisha ya watu. Lakini tunawezaje kupuuza nafasi ya siasa katika hili, ikiwa siasa za ghiliba ndizo zilizopachika viongozi wazembe wanaosababisha maafa yasiyokwisha kwa taifa?

Utakuwa ni ustaarabu wa kipuuzi ikiwa tutabaki kulialia tu na kuomboleza mauti yatokanayo na Serikali ya kizembe, bila kuchukua hatua za haraka dhidi ya serikali hii. Nani alijua kuwa baada ya maafa ya meli ya mv Bukoba, kungetokea tena maafa haya ya MV Spice Islanders? Nani alijua kuwa baada ya milipuko ya mabomu ya Mbagala, kungetokea tena maafa ya milipuko ya mabomu ya Gongo la Mboto? Nani anajua kuwa kabla ya mwaka 2015, Serikali hii hii ya kizembe, itakuwa imesababisha tena maafa na mauti mengine kwa Watanzania?

Na nani anajua kuwa katika maafa na mauti yajayo kizembe, mmoja wa marehemu anaweza kuwa mimi au wewe?

Badala ya kumsingizia Mungu, tuchukue hatua. Kama nchi imelaaniwa, basi ni muhimu ikafanyika toba ya kitaifa, ili atunusuru na uzembe na nuksi zote (kama zipo) zinazosababisha mauti makubwa kwetu. Kinyume na hayo, tunapaswa kuanzisha vuguvugu lisilokoma la kunusuru uhai wetu na wa nchi yetu dhidi ya utawala wa kizembe, na si lazima kusubiri uchaguzi wa 2015.

Mauti ya kizembe hayasubiri chaguzi, yanatokea wakati wowote na yanaweza kutuchukua sote, wewe mimi au wapendwa na wapenzi wetu. Pima mwenyewe…
Mungu wetu hana sababu ya kuhangaika kujaza mizigo mingi na abiria wengi kwenye meli ili izame ndipo aweze kuwachukua watu wake kwa kuchomoa roho zao.

Na wala hana sababu ya kuwaua watu wake kwa mv Bukoba halafu tena aje awaue kwa MV Spice Islanders. Hapana, yote hiyo ni kazi ya binadamu wazembe waliopewa dhamana ya kulinda uhai wa binadamu wenzao. Mungu wetu akitaka kukuchukua anakuchukua tu, si mpaka asubiri meli zijaze watu kupita kiasi au zipate hitilafu.

Watanzania wenzetu zaidi ya 240, kama mimi na wewe, wamepoteza uhai kwa sababu tu meli ya mv Spice Islanders ilipakia mizigo na abiria wengi kupita kiasi, au ilipata hitilafu, na hivyo kuzama kwenye Bahari ya Hindi. Isingepakia mizigo na abiria wengi isingezama, au ingekaguliwa vizuri na kufanyiwa matengenezo ya kufaa kabla ya safari, isingepata hitilafu wala kuzama.

Kwa maana hiyo, maafa yaliyotokea yangeweza kabisa kuepukika kama vyombo vya Serikali hii, ikiwemo mamlaka za usafiri wa majini, vingekuwa vinatimiza wajibu wake bila kuzembea.

Itiliwe maanani kuwa meli hiyo ilizama majira ya saa 7 usiku, na abiria wengi walikuwa wakifanya jitihada za kujiokoa, lakini kwa sababu ya “uzembe”, vikosi vya uokoaji vilichelewa kutumwa eneo la tukio na matokeo yake vilifika saa 12 asubuhi, takriban saa tano baada ya ajali kutokea.Katika hali hiyo, abiria wengi ambao wangeweza kuokolewa walikuwa wameshapoteza maisha.

Katika moja ya maandiko yake kuhusu “Uzembe wa Serikali ya CCM”, Mwanaharakati, Erick Ongara, baada ya kutokea kwa maafa ya milipuko ya mabomu ya Gongo la Mboto, aliandika hivi, namnukuu kwa kirefu:
“Tunaandika kwa hisia nzito sana. Tumefikishwa mahala ambapo tunalazimika kuwalinda raia dhidi ya Serikali yao. Ni kama kuwatenganisha vitoto vya mnyama wa kufuga na Mzazi wao ili kuwaokoa wasiliwe. Serikali ya CCM ikitumia silaha yake kubwa ya maangamizi iitwayo “uzembe” imeua waajiri wake kwa mara nyingine tena.

Imewaua, ikawalemaza, ikaharibu mali zao na kuwapa athari hasi na za kudumu Watanzania huku ikiendelea kuwafukarisha. Serikali ya CCM imejingea utamaduni wa kuishi katika duara la uzembe. Yaani huwa inahaidi, haijali, haijifunzi, haitendi na inapumzika mda wote kisha duara la uzembe linaanza tena.

Baada ya maafa ya Mbagala, serikali ya CCM ilihaidi kwamba hali hii haitatokea tena, kisha haikujali kufuatilia ilichoahidi, haikutenda katika kudhibiti uwezekano wa hali hiyo kujirudia na hatimaye ikapumzika. Baada ya mwaka mmoja na nusu duara la uzembe lilianza tena na kusababisha milipuko ya mabomu kutokea kwenye kambi ya jeshi Gongo la mboto.

Gongo la Mboto imeshalipuka na tayari wameahidi, kisha hawatajali, hawatatenda, watapumzika na hatimaye wataua tena kwa staili nyingine ya kizembe na duara la uzembe litaanza tena mwanzo.

Mwaka 2006 taifa lilikuwa na changamoto kubwa sana ya umeme. Wakasema tuna dharura. Wakabuni kampuni ya uongo. Wakajilipa, wakatunga kesi,wakahakikisha wanashindwa na sasa wanataka tuilipe fidia kampuni hiyo.

Leo duara la uzembe limeanza tena. Kuna dharura ya kuliokoa taifa dhidi ya kiza totoro.

Baada ya mwaka 2006, waliahidi, hawakujali, hawakutenda,wakapumzika na leo tumerudi pale pale. Tuna dharura (wamekuja na mpango wa dharura).

Kwa serikali hii ya kizembe, Tanzania ndiyo imekuwa taifa pekee dunia, lenye dharura za kudumu.

Kinachoumiza, vifaa vinavyopaswakuwalinda raia ndivyo vinavyowaangamiza. Risasi za polisi wa Arusha zilipaswa kuwahakikishia ulinzi raia, lakini zikawaua kwa kuwa tu walikuwa wanatembea pamoja wakiwa wameshika vitambaa vyeupe.

Wakazi wa Mbagala na Gongo la Mboto wamepoteza maisha kwa mabomu ambayo yalipaswa kuwahakishia ulinzi. Wanakatwa kodi, silaha zinanunuliwa kisha zinaingizwa katika mfumo wa duara la uzembe. Wanaahidi, hawajali, hawatendi na hatimaye wanapumzika.

Kwa bahati mbaya sana umma nao una duara saidizi kwa duara la uzembe. Kuna duara la uovu. Serikali inapokosea na kushindwa kutekeleza wajibu wake katika kiwango cha kuhatarisha na hata kupokonya maisha yao, Watanzania huwa tunajadili, tunachambua, tunalalamika, hatuchukui hatua kisha tunapumzika.

Serikali ikilizua tena, huanza duara upya, wananchi watajadili, watachambua, watalalamika, hawatachukua hatua kisha watapumzika, na matokeo yake maafa mengine yataibuka tena kwa sababu ya uzembe.

Zipo sauti zinazotaka mkuu wa majeshi na waziri wa ulinzi wajiuzulu kama sehemu ya uwajibikaji. Ni kweli na ni sawa kwa kuwa ndio wao walioahidi,kisha hawakujali,hawakutenda na hatimae wakapumzika.

Ili kudhoofisha duara hatari la uzembe lazima waaachie ngazi kwa maana wameshindwa kubeba dhamana ya kulinda uhai wetu.

Lakini hiyo pekee haitoshi. Lazima kutokomeza kabisa duara la uzembe kwa kumwajibisha kiongozi wa juu anaelea duara hili (Rais wa Nchi).

Ili kuondoa duara la uzembe lazima kwanza tuondoe duara la uovu.Watu wa Misri hivi karibuni hawakutengeneza duara bali mstari. Walichambua, wakakubaliana, wakajikusanya, wakashinikiza na hatimaye kuvunja duara la maangamizi kwao, ambalo lilidumu kwa miongo kadhaa.

Tumeumia sana na tunawapa pole ndugu zetu kwa maafa wanayoyakabili. Inawezekana, timiza wajibu wako. Mwisho wa kunukuu.

Baada ya maafa ya milipuko ya mabomu Gongo la Mboto, duara la uzembe liliendelea tena, na serikali ya CCM ambayo wakati wa ajali ya mv Bukoba, iliahidi kuongeza usalama wa vyombo vya usafiri wa majini, ikafanya tena uzembe na kusababisha meli ya mv Spice Islanders kuzama baada ya kuiacha ipakie mizigo na abiria wengi kupita kiasi. Na sasa taifa linaomboleza msiba mzito, msiba wa kizembe.

Katika hali hii ya ajali za kizembezembe, ni dhambi kubwa kusema “ajali haina kinga”, au kusema “kazi ya Mungu haina makosa”. Mungu wetu si mzembe. Kwa serikali hii, daima tutaomboleza mauti ya kizembe. Ni wakati wa kuchukua hatua za haraka. Tutafakari kwa pamoja.

SOURCE: Tanzania Daima Newspaper, September, 2011

No comments:

Post a Comment