Thursday, December 22, 2011

Maaskofu, Mapadri washambuliwa

Na Edward Kinabo,

VIONGOZI wa dini wakiwemo baadhi ya maaskofu, mapadri na wachungaji wa madhehebu mbalimbali ya kikristu nchini, wameaswa kuacha tabia ya kuwatanguliza mbele wanasiasa katika kila shughuli ya kiroho wala kuzigeuza nyumba za ibada kuwa vijiwe vya kuwasafisha na kuwahalalisha watu wenye malengo binafsi ya kutafuta uongozi.

Tuhuma na ushauri dhidi ya viongozi wa dini nchini zilitolewa jana na Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alipozungumza na waandishi wa habari mjini hapa, kutoa salaam zake maalum kwa viongozi wa dini kuelekea sikuu kuu za X mas na mwaka mpya wa 2012.

Msigwa alisema katika mwaka unaomalizika wa 2011 kulishamiri desturi ya baadhi ya wanasiasa hususan wale wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kupenda kuwatumia vibaya baadhi ya viongozi wa dini na nyumba za ibada kama sabuni ya kujisafisha na ngazi ya kufikia malengo ya kuutafuta urais au ubunge na udiwani.

Alisema ingawa Kanisa ni mahali pa kusafishwa uchafu na kila mtu anakaribishwa, lakini pia si sahihi kwa kanisa au nyumba nyingine za ibada kutumika kusafisha watu kwa malengo yao ya kibinafsi.

“Ingawa kanisa ni mahali pa kusafishwa uchafu na kila mtu anakaribishwa, lakini tumkumbuke yule Simon Mchawi katika kitabu cha matendo ya mitume,aliyejaribu kununua kipawa cha Roho mtakatifu kwa faida yake binafsi, ndipo mtumishi wa Mungu Petro alipomwambia apotelee mbali pamoja na pesa yake”, alisema Mchungaji Msigwa.

Aliwataka viongozi wa dini wenzake wasikubali kamwe kuwa mawakala wa kufanikisha kile alichokiita “mbio za urais mchafu”, wala kuwa chini ya wanasiasa, kwani jukumu la viongozi wa dini kwa binadamu ni zito na kubwa kuliko uroho wa madaraka aliodai kuwa ndio unaowakimbiza baadhi ya wanasiasa kwenye nyumba za ibada.

“Kanisa likitakiwa kuzinduliwa, mwanasiasa, uzinduzi wa nyimbo ya injili, mwanasiasa, ununuzi wa magitaa, mwanasiasa, ununuzi wa maspika, mwanasiasa. Hivi hawa wanasiasa wana upako gani kana kwamba kazi ya Mungu haiwezi kufanyika bila wao?

Sisi viongozi wa dini tunapaswa kuwa viongozi na sio wafuasi wa wanasiasa, tunapaswa kuwaonyesha njia wanadamu wote wakiwemo wanasiasa na sio wanasiasa watuonyeshe njia sisi, maana kufanya hivyo ni kulishusha thamani neno la Mungu”, alisema

Ingawa hakuwataja kwa majina baadhi ya wanasiasa wa CCM aliodai wanakimbilia makanisani kutafuta madaraka, lakini Edward Lowassa (Mbunge wa Monduli), Samuel Sitta (Waziri Afrika Mashariki) na Bernard Membe (Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa), ndio wamekuwa wakionekana zaidi kwenye matukio ya kanisa huku matukio hayo yakihusishwa na mbio za urais 2015.

“Ni udhalilishaji mkubwa wa huduma ya kiroho pale sisi viongozi wa dini tunapowatanguliza wanasiasa kwenye kila shughuli kama ya uzinduzi wa makanisa au albamu za nyimbo za kidini, kana kwamba wanasiasa ndio wenye upako, utukufu na mamlaka zaidi ya kubariki kinachozinduliwa kuliko sisi viongozi wa dini wenyewe.

“Tusikubali nyumba takatifu za ibada zigeuzwe viwanja vya kampeni za kisiasa na wala tusiwe chanzo cha kuiingiza nchi yetu katika mgawanyiko na machafuko ya kidini kwasababu tu ya kuwabeba baadhi ya wanasiasa ambao ama kwa sababu ya uchafu wao au umma kukosa imani nao, wameona hawawezi tena kuwa na uhalali wa kujitangaza wala kujijenga tena kwenye majukwaa ya kisiasa bila kwanza kukimbilia makanisani”, alisema Mbunge huyo na kuongeza:

“Binafsi naamini, mwanasiasa msafi anayejiamini na anayemcha Mungu kwelikweli haitaji harambee au tukio lolote la kujinadi kanisani , maana huko si pahali pake”

Alisema anafahamu kuwa taifa kwa ujumla wake lina hali duni kimaisha zinazowagusa pia viongozi wa kiroho, lakini hali hiyo isiwafanye baadhi ya viongozi wa dini kusahau misingi yao ya kitume kana kwamba Mungu aliyewaita amewaacha.

“Tunapokwenda kusherehekea siku kuu hii ya X Mas na Mwaka Mpya, ninawasihi tena viongozi wenzangu wa kidini, kwamba tumkumbuke mtumishi wa nabii Elisha, aliyeitwa Gehazi, ambaye alipenda pesa na zawadi akasahau mwito wake wa kitume mpaka ukoma wa Nahaman ukahamia mwilini mwake.

Na tumkumbuke Yuda Eskarioti ambaye alimuuza mwokozi wetu, Yesu Kiristu, kwa vipande thelathini vya fedha, na kwa hiyo, sisi viongozi wa dini tusikubali kamwe kuwauza Watanzania wenzetu kwa pesa za wanasiasa wachafu”, alisema mbunge huyo ambaye pia ni mchungaji wa kanisa la Vineyard.

Alisema anamini kuwa viongozi wa dini wakisimama imara bila kuyumba, Tanzania inayougua umaskini, ujinga, maradhi na ufisadi, hatimaye itaponywa.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment