Na Edward Kinabo
UHALALI wa Rais Jakaya Kikwete kuwa madarakani unazidi kutia shaka baada ya ripoti ya mwisho ya waangalizi wa Umoja wa Ulaya kutoa maelezo yanayothibitisha kuwapo kwa mwanya mkubwa wa kura kuibiwa na matokeo kubadilishwa katika uchaguzi mkuu wa Rais uliofanyika mwaka jana (2010).
Wakati Rais Kikwete na chama chake walidai kura zisingeibiwa kwa sababu kila chama huruhusiwa kuweka wakala wake, ripoti hiyo ya ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi mkuu kutoka Jumuiya ya Ulaya (EU) inawaumbua, baada ya kueleza waziwazi bila kumung’unya maneno kwamba mawakala wa vyama vya siasa na waangalizi wa uchaguzi hawakuruhusiwa kushuhudia ujumlishaji wa matokeo ya uchaguzi wa rais.
Ujumbe wa waangalizi hao wa EU ukiongozwa na Mbunge wa Bunge la Ulaya, David Martin, ulikuwepo nchini tangu Septemba 29 hadi Novemba 28 mwaka jana na ulisambaza waangalizi wake 103 katika mikoa yote 26 ya Bara na Visiwani.
Katika ripoti hiyo ambayo Tanzania Daima Jumapili inayo nakala yake, wataalamu hao wameeleza kuwa matokeo ya kura za urais mwishowe yalijumlishwa na viongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wakiwa peke yao bila kushuhudiwa na mawakala wa vyama vya siasa, utaratibu ambao kwa mtazamo wa kawaida, ulitoa mwanya mkubwa kwa kura kuibiwa au matokeo halali kubadilishwa, huku ukiwepo uwezekano wa Kikwete kupendelewa kwa sababu ya kile kinachofahamika kuwa ndiye aliyewateua kuiongoza tume hiyo kwa mamlaka yake ya uteuzi kama rais.
“Matokeo ya uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Muungano yalijumlishwa na makamishna wa NEC. Matokeo ya kila jimbo la uchaguzi yalitumwa Idara ya Teknolojia ya Habari ya NEC (NEC IT Department) kwa njia ya kompyuta, ambapo yalipokewa na makamishna wa NEC.
Mawakala wa vyama vya siasa na waangalizi wa uchaguzi hawakuruhusiwa kufuatilia ujumuishaji wa matokeo ya uchaguzi wa rais”, ilisema ripoti hiyo yenye kurasa 61.
Wakizidi kuonyesha jinsi ujumlishaji wa kura za urais ulivyogubikwa na usiri mkubwa uliokuwa na nia mbaya, wataalamu hao katika ukurasa wa 51 wa ripoti yao, wanasema:
“Licha ya kuwapo hakikisho la waangalizi wa uchaguzi kuruhusiwa kuwepo kwenye hatua zote za uchaguzi, ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Ulaya (EU EOM) haukuruhusiwa kuwepo kwenye hatua muhimu za michakato ya ujumlishaji na uthibitishaji wa matokeo, hususan matokeo ya uchaguzi wa rais.”
Wakizungumzia zaidi mfumo wa usiri uliotumika kujumlisha matokeo na ulivyoweza kuathiri uhalali wa matokeo yenyewe, waangalizi hao wamesema: “Taratibu za kuhesabu na kujumlisha matokeo katika ngazi ya kituo cha kupigia kura; wilaya na taifa maelezo yake ingefaa yatolewe wazi moja kwa moja kwenye kifaa ambacho yanaweza kurekodiwa na kuonyeshwa, kisha kuonekana wazi kwa macho kwa wadau wote. Kufanya hivyo, kungedumisha uhalali wa matokeo na uwazi wa tume ya uchaguzi”.
Ikigusia mwenendo wa kampeni na matumizi ya rasilimali za serikali, ripoti hiyo imeonyesha jinsi vyombo vya habari vya serikali vilivyoripoti zaidi kampeni za CCM na chama hicho kunufaika na muundo wa kiutawala kuliko vyama vya upinzani, huku ikibainisha kuwa vyama vya upinzani havikukata tamaa ya kushindana kutokana na hali hiyo.
“Chama kikuu cha upinzani cha CHADEMA upande wa Bara, taratibu kilizidi kuungwa mkono baada ya kipindi kirefu cha kampeni,” ripoti hiyo inasema.
Pia wachunguzi hao wanasema kutokana na kuwepo kwa dosari nyingi kwenye mchakato wa kujumlisha matokeo ya uchaguzi wa rais kwenye baadhi ya majimbo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kiliandikisha lalamiko NEC Novemba 4, mwaka jana na kuitaka isitishe kutangaza matokeo na badala yake irudie upya uchaguzi, lalamiko ambalo hata hivyo lilitupiliwa mbali na NEC, ambayo ilidai kuwa tuhuma zilizotolewa zingepaswa kuwasilishwa kwa wasimamizi wa kura.
Katika ukurasa wa 55 wa ripoti hiyo, waangalizi hao wamependekeza kuanzishwa kwa haki ya matokeo ya uchaguzi wa rais kupingwa mahakamani.
Kwa upande mwingine ripoti hiyo imeeleza kile kinachoonekana kuwa ni busara na hekima aliyoonyesha Dk. Slaa kwa kukataa kutoa mwito kwa wananchi kufanya vurugu baada ya kutoridhishwa na matokeo ya urais.
“Dk. Slaa hakutoa mwito wowote wa kufanya vurugu au kuuchochea mjibizano ulioratibiwa na wafuasi wa chama chake, bali alitaka kuwe na uchaguzi mpya wa urais wa Jamhuri ya Muungano kwa manufaa na faida ya taifa zima kutokana na matokeo ya uchaguzi yaliyotolewa na NEC kutodhihirisha matakwa ya wapiga kura,” ilifafanua zaidi ripoti hiyo.
Gazeti hili liliwahi kuandika taarifa nyingine za uchunguzi zilizokuwa pia kwenye mitandao ya kompyuta (internet) zilizoeleza kuwa Dk. Willibrod Slaa aliyekuwa mgombea urais kupitia CHADEMA alishinda uchaguzi huo kwa kupata asilimia 64 ya kura zilizopigwa.
Taarifa hizo zilieleza kuwa matokeo zaidi ya urais yalichakachuliwa katika majumlisho ya mwisho ya kura nchi nzima, ambapo NEC inadaiwa ilipunguza kura za Dk. Slaa hata zile zilizokuwa zimeshuhudiwa kwa pamoja na mawakala wa vyama vya upinzani katika ngazi za majimbo.
Hata hivyo kama ilivyotarajiwa, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Lewis Makame, alikanusha vikali taarifa za Dk. Slaa kushinda urais kupitia gazeti la Uhuru linalomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
No comments:
Post a Comment