Monday, October 24, 2011

Waraka wa Kinabo:Ufunuo wa Chadema Musoma

Na Edward Kinabo

MAENDELEO ya kweli na ya haraka yanawezekana, ikiwa kuna serikali yenye viongozi waadilifu na wanaojituma kwa dhati kuwatumikia wananchi.

Ndani ya kipindi cha takriban miezi tisa tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2010, Serikali mpya ya Manispaa ya Musoma Mjini imethibitisha ukweli huu licha ya changamoto nyingi zilizopo.

Serikali hii imeundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), baada ya kushinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. Meya, naibu meya na wenyeviti wote wa kamati za halmashauri, ikiwamo Kamati ya Fedha, Ardhi na nyinginezo, wote wametoka CHADEMA.

Hii ni kwasababu wananchi mbali na kuchagua mbunge kutoka CHADEMA (Vincent Nyerere), pia walikipa chama hiki maarufu mjini hapa kwa jina la “People”, madiwani wengi (11) huku CCM ikiambulia madiwani (4) na CUF (3).

Ziara yangu ya kiudadisi na kiupembuzi ilinikutanisha na wananchi wa kata mbalimbali za mjini Musoma, vijana, wazee na akina mama kwa kadiri nilivyoweza, ambapo kutoka kwao niliweza kupata taarifa na maoni huru kuhusu hali halisi ya wilaya yao ndani ya kipindi hicho kifupi cha miezi tisa. Aidha, iliniwezesha kutembelea na kushuhudia mafanikio yote ya kuonekana kwa macho, niliyoelezwa na wananchi.

Na hatimaye niliweza kupata taarifa za kitakwimu kutoka kwa Meya wa Mji huu, Alex Kisurura, Mbunge, Vincent Nyerere, pamoja na madiwani na baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa bila kujali vyama vyao. Ziara hii ilinionyesha mambo kadhaa ya kupigiwa mfano yaliyopatikana ndani ya kipindi hicho kifupi tangu CHADEMA waingie madarakani, kama ifuatavyo:

Kwanza, kwa mtu aliyefika Musoma Mjini mwezi Oktoba mwaka jana (kabla ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu), halafu akaingia tena hivi sasa, tofauti ya Serikali ya CCM iliyokuwepo na hii mpya ya CHADEMA inaonekana wazi wazi katika barabara za mitaa ya mji huu. Barabara nyingi kama za Kata ya Bweri, Nyamatare, Nyasho, Makoko, Mwisenge, Kigera na Buhare (eneo la Bima quarters) zilikuwa hazipitiki, na za kata nyingine chache zilipitika kwa tabu kwa sababu ya mashimo na makorongo mengi, lakini sasa zote zinapitika baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa na kuwekewa mitaro ya kupitishia maji pembeni ambayo haikuwepo kabisa, hivyo kuhakikisha haziharibiki mara kwa mara.

Katika elimu, serikali ya CHADEMA ilipoingia madarakani ilifanikiwa kufuta michango mingi isiyo ya lazima na kuipunguza ile iliyokuwa na umuhimu, ili kumpunguzia mwananchi mzigo wa gharama. Michango hiyo ambayo wakati wa utawala wa CCM ilifikia kiasi cha shilingi 140,000 hadi 250,000 kwa kila mwanafunzi, hatimaye imepunguzwa hadi kufikia wastani wa shilingi 52,000 hadi 62,000 tena pale tu kunapokuwa na ulazima.

Mathalani, mchango wa madawati uliokuwa shilingi 50,000 kwa kila mwanafunzi, lakini umepunguzwa hadi shilingi 5,000. Mbali na punguzo hilo, serikali ya CHADEMA pia ilichukua jukumu la kukarabati madawati kwenye shule zote za msingi. Na mchango wa maendeleo ya taaluma umepunguzwa kutoka shilingi 40,000 hadi shilingi 10,000.

Pia shule mpya (Shule ya Msingi Bukanga) imeanzishwa, ili kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu watoto wa eneo la Bukanga ambao wakati wa utawala wa CCM, walikuwa wanalazimika kutembea umbali wa takribani kilometa tatu kuifuata Shule ya Msingi Nyarigamba. Shule hiyo imeshaanza darasa la kwanza na inatumia majengo ya muda, huku ujenzi wa majengo yake ukisubiriwa kukamilika.

Na zipo shule nyingine tano za msingi ambazo zinajengewa maabara kwa fedha za Mfuko wa Jimbo. Sehemu ya fedha za mfuko huo pia inatumika kumalizia ujenzi wa majengo ya Sekondari kwenye Kata 10, ambayo Serikali ya CCM ilishindwa kuyakamilisha. Baraza la Halmashauri hii pia limeshaanza kutekeleza mpango wake wa kuzifanya sekondari za Morembe na Kyara kutoa elimu ya kidato cha tano na cha sita.

Viongozi wa CHADEMA pia wanawasomesha watoto yatima na wasiojiweza wilayani hapa kwa kuwalipia ada na gharama nyingine za elimu. Katika utaratibu huo waliojiwekea, Mbunge Nyerere, anasomesha watoto 70, Meya Kisurura watoto 100 na madiwani wa CHADEMA nao wana watoto wasiojiweza wanaowasomesha kwa fedha zao wenyewe. Kwa ujumla, kuna watoto wasiojiweza zaidi ya 200 wanaogharamiwa masomo na viongozi wa CHADEMA. Mbali na idadi hiyo, Serikali hii pia iliamua kuanza kuwalipia ada watoto 100 wasiojiweza, ambao serikali ya CCM iliwatelekeza kwa kuacha kuwalipia ada tangu mwaka 2008.

Katika nyanja ya afya, wananchi wa Musoma Mjini pia wana kitu cha kujivunia kwa kuiweka CHADEMA madarakani. Kwa kauli zao wenyewe na kwa ushuhuda wa macho na utashi wangu, ndani ya kipindi hicho kifupi tayari wodi ya watoto katika Zahanati ya Nyakato inajengwa na bado kidogo kukamilika.

Na chini ya usimamizi wa serikali hii, wodi kama hiyo pia inajengwa katika Zahanati ya Kigera kwa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Kwa mara ya kwanza katika manispaa hii, wazee, watoto walio chini ya miaka mitano na kina mama wajawazito wanatibiwa bure katika hospitali za serikali hapa Musoma.

Na Serikali hii ya CHADEMA imeshaanza kutayarisha vitambulisho kwa watu wa makundi hayo, ili kuhakikisha kuwa wanapata haki hiyo ya kutibiwa bure katika siku zote za maisha yao, haki ambayo walikuwa hawaipati wakati wa utawala wa CCM, licha ya sera za kiserikali kutamka hivyo.

Zahanati mpya zinaendelea kujengwa kwa kasi katika kata za Iringo na Buhare, pamoja na kuweka uzio kwenye Kituo cha Afya cha Nyasho na kwenye zahanati ya Bweri.

Kwa sababu ya ufisadi na usimamizi mbovu wa Serikali ya CCM, miradi mingi ya TASAF wilayani hapa kwa muda mrefu ilishindwa kukamilika na kubaki kusuasua, lakini sasa hali ni tofauti. Tayari ujenzi wa Zahanati ya Nyamatare uko mbioni kumaliziwa baada ya fedha za mradi huo kupatikana.

Aidha, msukumo wa Mbunge Nyerere na madiwani umewezesha kupatikana kwa gari jipya la kisasa la kubebea wagonjwa mahututi (Ambulance) kwa ajili ya kuwapeleka kwenye hospitali kubwa jijini Mwanza, huku mpango wa kufufua na kukamilisha ujenzi wa Hospitali Kuu ya Mkoa wa Mara, uliosuasua kwa miaka mingi mjini hapa, ukishughulikiwa kwa kasi.

Na katika hili, jitihada za Nyerere zimesaidia baadhi ya familia zilizohamishwa kwenye eneo linalojengwa hospitali hiyo, kulipwa fidia ya jumla ya shilingi milioni 100, ambayo walikuwa wakiidai kwa muda mrefu bila mafanikio.

Wakati wa utawala wa CCM wakazi wa Musoma Mjini walikuwa wakiteseka kwa shida kubwa ya maji, licha ya kuwa mji huu umezungukwa na Ziwa Victoria.

Hii ni kwasababu, kwa zaidi ya miaka 30, Serikali ya CCM haikufanya kazi ya kukarabati miundo mbinu ya mabomba ya maji, ambayo sasa imechakaa kiasi cha kuwa na uwezo wa kusambaza maji kwa wananchi 50,000 tu, wakati Musoma yenyewe ikiwa inakadiriwa kuwa na watu takriban 181,000. Serikali mpya imeamua kulishughulikia kwa kasi tatizo hili linalogusa moja kwa moja uhai wa binadamu, na sasa mradi wa maji utakaogharimu takriban shilingi bilioni 50 unaanza kutekelezwa chini ya usimamizi wake.

Wakati mradi huo mkubwa ukianza, baraza la halmashauri limekwisha kuidhinisha fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kupeleka maji kwenye Kata ya Buhare, iliyo katika shida kubwa. Na tayari mpango wa uchimbaji wa visima vya dharura hivi karibuni upo mbioni kuanza, hususan kwenye maeneo yenye shida kubwa sana ya maji kuliko maeneo mengine. Mipango ya mbunge, meya na madiwani, ni kuhakikisha shida hii inakwisha kabisa katika maeneo yote kwani maji ya Ziwa Victoria yapo, kazi iliyoishinda CCM ni kuyavuta tu.

Katika nyanja ya ajira, kwanza serikali ya CHADEMA ilipoingia tu madarakani hapa Musoma, ilifuta ushuru uliokuwa ukitozwa kwa wafanyabiashara ndogondogo za uchuuzi kama ule uliokuwa ukitozwa kwa kina mama wanaouza mbogamboga, matunda, dagaa na bidhaa nyingine ndogondogo za kujitafutia riziki, lengo likiwa ni kuwapa nafuu ya maisha wananchi hawa.

Pili, kwa lengo la kuwajengea wananchi mazingira mazuri ya kujipatia kipato, serikali hii imeweza kukarabati na kulifufua Soko la Kamnyonge ambalo lilisimama tangu mwaka 1986.

Masoko mengine yanayofuatia katika mpango huo, ni Soko Kuu la Musoma, Soko la Mlango Mmoja, Nyasho, Soko la Samaki (Makoko), Nyakato na Soko la Mwalo wa Mwigobero ambalo litaanza kukarabatiwa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Bandari Tanzania.

Tatu, vijana waendesha pikipiki (bodaboda) waliokuwa wanalalamikia utaratibu wa kulipa kodi ya shilingi 95,000 kwa mkupuo mmoja kwa mwaka, sasa wamepewa nafuu ya kutakiwa kulipa kodi hiyo kidogokidogo, ilimradi tu mwaka usiishe bila mhusika kukamilisha malipo ya kiwango hicho cha kodi.

Nne, vibanda vya biashara vya manispaa hii vilivyokuwa vinamilikiwa na watu wachache wakati wa CCM, sasa vimetaifishwa na serikali ya CHADEMA na kugawanywa kwa usawa kwa wananchi wengi zaidi wakiwemo walemavu, ili kuwapa fursa ya kujitafutia mkate wao wa kila siku.

Tano, serikali hii mpya pia inasimamia ujenzi na upanuzi wa stendi kuu ya mabasi makubwa yaingiayo Musoma (Stendi ya Bweri), ili iweze kufanya kazi kwa saa 24 na kwa ufanisi zaidi na hivyo kuipatia manispaa mapato ya kutosha kwa ajili ya miradi mingine ya maendeleo, na wakati huo huo ikitazamiwa kutoa fursa nzuri kwa wajasiriamali wa mji huu kujitengenezea kipato kwa kufanya biashara.

Sita, nimeshuhudia kukamilika kwa ujenzi wa kivuko kikubwa ambacho kitafungua safari za ziwani kutoka Musoma hadi Bunda. Mradi huu unatarajiwa kuchochea maendeleo ya shughuli za kibiashara na kiuchumi baina ya wilaya hizi mbili zinazozungukwa na Ziwa Viktoria.

Saba, serikali hii imeamua kuwa asilimia 10 ya mapato ya manispaa yanayopaswa kushughulikia maendeleo ya vijana na kina mama, yatumike kuanzisha miradi midogomidogo ya pamoja, badala ya kutoa mikopo isiyo na tija ya shilingi elfu 50 kwa mtu mmoja mmoja.

Kwa mujibu wa viongozi wa serikali hii, baadhi ya miradi ambayo iko mbioni kubuniwa kwa kuwashirikisha wananchi wenyewe ni pamoja na kuanzisha kiwanda kidogo cha kutengeneza biskuti za viazi, ununuzi wa mashine za kutotolea vifaranga, kutengeneza chakula cha kuku, kutengeneza chaki, na kuviwezesha baadhi ya vikundi vya wavuvi na wafugaji kuuza samaki na maziwa ya kutosha kwenye viwanda viwili vilivyopo mjini hapa.

Katika nyanja ya utawala bora, meya, mbunge na madiwani wa manispaa hii, wamejiwekea utaratibu wa kufanya mikutano ya hadhara ya mara kwa mara na wananchi ili kuwapa mrejesho wa kazi wanayoifanya na kupokea kero na matatizo mapya kutoka kwao. Pia viongozi hawa kila mmoja ameshawatangazia wananchi namba yake ya simu ya mkononi, kwa ajili ya kutoa kero na matatizo yao kwa urahisi ili yapatiwe ufumbuzi wa haraka.

Na wakati huo huo serikali hii inaendelea kujenga ofisi za watendaji kata, ambazo hazikuwepo kwenye kata mbalimbali mjini hapa ili zitumiwe na wananchi kama fursa ya kuwasilisha kero, matatizo na malalamiko yao kwa diwani, mbunge au halmashauri yote.

Viongozi wanahakikisha kuwa asilimia 20 ya fedha za mapato ya manispaa inabaki kwenye ofisi za serikali za mitaa, ili kuhakikisha kuwa ofisi hizo zinawahudumia wananchi bila kuwatoza chochote. Kabla ya hapo ulikuwa huwezi kupata barua ya utambulisho kutoka ofisi ya mtaa, au kutatuliwa mgogoro wako, bila kuchangia fedha kama shilingi 2,000 ya karatasi au fedha za kuwaita wajumbe kwenye vikao vya usuluhishi (michango hii haramu bado ipo maeneo mengi nchini ikiwemo kwenye ofisi za serikali za mitaa za jijini Dar es Salaam).

Nilipata bahati ya kupitia pia ripoti mbalimbali za kifedha kuhusu manispaa hii, kubwa nililobaini ni kwamba serikali hii mpaka sasa imeshafanikiwa kudhibiti matumizi makubwa na ya anasa ya fedha za umma.

Mathalani, idadi ya semina, warsha na safari za nje ya manispaa zilizokuwa zikifanywa na meya, naibu meya na madiwani wa CCM wakati wa enzi za utawala wao, sasa zimedhibitiwa kwa kiasi kikubwa, na badala yake fedha hiyo nyingi ndiyo inayotumika kutekeleza kwa kasi miradi mingi ya maendeleo ya wananchi.

Changamoto zipo nyingi ikiwemo ya uhaba wa fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo, lakini bado serikali hii inaonekana kufanya mengi ya kuvutia ndani ya kipindi kifupi tu cha miezi tisa.

“Tulipokea mji huu ukiwa katika hali mbaya sana. Wakati CCM imetumia miaka 50 kufanya vitu vichache na visivyoonekana dhahiri, sisi mpaka sasa tumeweza kufanya vitu vingi ndani ya miezi nane tu, na bado tuna uhakika wa kufanya makubwa zaidi ndani ya miaka mitano.

Siri ya mafanikio haya, ni uadilifu, uwajibikaji na kutekeleza kwa vitendo falsafa ya CHADEMA ya “nguvu ya umma”, ambapo kwa falsafa hiyo, tumeweza kuiweka serikali hii mikononi mwa wananchi wenyewe, kwa kuwafanya kuwa ndio waamuzi wa mwisho wa nini wanataka kifanyike, huku tukiwapa fursa ya kufuatilia na kusimamia kila kinachofanyika.” (Kauli ya Vincent Nyerere).

Hakika huu ndio ufunuo wa CHADEMA kwa Watanzania kutoka Musoma, kwamba, “Maendeleo yaliyoshindikana ndani ya kipindi kirefu cha ufisadi, uzembe na usanii, sasa yanawezekana ndani ya kipindi kifupi cha uadilifu, na uwajibikaji”.

SOURCE: Tanzania Daima Newspaper- Wednesday October 19, 2010

No comments:

Post a Comment