Friday, December 2, 2011

Aya za Ukombozi: Kutoka uchaga hadi ukatoliki, tuwaeleweje?

WIKI chache kabla ya kuanza rasmi kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani, nawasilisha aya hizi kuvikumbusha vyombo vya habari kuwa havipaswi kufungamana na chama wala wagombea, lakini wakati huo huo kila chombo cha habari kina haki na wajibu wa kupinga na kulaani jitihada zozote za makusudi zinazofanywa na watu au chombo kingine cha habari, zenye lengo la kuchonganisha, kuchochea au kupandikiza chuki na ubaguzi wa aina yoyote ile dhidi ya Mtanzania yeyote yule, iwe ni dhidi ya mwanasiasa au mwananchi wa kawaida.

Nikiitumia safu ya ‘Waraka wa Kinabo’, nimewahi kukemea na kulaani uchochezi na ubaguzi wa kidini na kikabila kuwa ni hatari kwa umoja na mshikamano wa taifa na hatari kwa amani na maendeleo yetu lakini hali hiyo imekuwa ikiendelezwa kwa makusudi.

Leo nimelazimika tena kuurudia wajibu wangu huo, baada ya kuona siasa hizo chafu zikitamalaki kwa kasi kubwa kutoka kwa wanasiasa ucharwa hadi kufikia kubebwa na baadhi ya vyombo vya habari vilivyojipatia heshima kubwa miaka ya nyuma kwa kuelimisha jamii na sasa kuonekana kubadilika na kutoa baadhi ya habari zinazoonekana dhahiri kuipotosha jamii.

Ndani ya kipindi cha takriban wiki mbili sasa tangu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbrod Slaa, akubali na kutangazwa kugombea urais kupitia chama hicho, kumekuwa na habari zinazoonekana dhahiri kuandikwa kimkakati (propaganda) zikilenga kuushawishi umma umbague mwanasiasa huyo kwa sababu ya dini na dhehebu lake.

Mfano mkubwa wa habari hizo ni ile iliyoandikwa na gazeti moja wiki iliyopita ikitaarifu kuwa wabunge Waislamu wa CHADEMA waliamua kususia mikutano ya Dk. Slaa anayoifanya kutafuta udhamini maeneo mbalimbali nchini kwa madai ya kuchukizwa na mgombea huyo kutumwa na maaskofu kugombea urais.

Tukiitazama kwa umakini habari hiyo tutabaini kuwa gazeti husika liliamua kwa makusudi kuwaandika wabunge hao wa CHADEMA kwa kutazama na kutumia zaidi kigezo cha dini zao (Waislamu) kuliko sababu za msingi zilizowafanya wakosekane kwenye mikutano hiyo.

Izingatiwe kuwa mmoja wa wabunge ambaye hakuwepo, Zitto Kabwe, alihojiwa na kukijibu chombo hicho kwamba kutokuwepo kwao kwenye mikutano hiyo kulisababishwa na wao kuwa na ratiba majimboni mwao lakini katika kile kinachoonekana ni kulazimisha na kukoleza chuki na ubaguzi wa kidini dhidi ya Dk. Slaa, chombo hicho kiliichapa habari hiyo huku kichwa cha habari na maudhui yake vikionekana dhahiri kuupa nafasi kubwa na kuupambanisha kwa makusudi Uislamu wa wabunge hao dhidi ya Ukiristu wa Dk. Slaa bila sababu za msingi.

Pasipo shaka yoyote ile, nathubutu kuthibitisha kuwa huu ni uchochezi unaopaswa kuchukuliwa hatua na mamlaka husika, si kwa kusubiria hadi aliyeguswa alalamike kwa Waziri wa habari au Baraza la Habari, bali kwa mamlaka husika kuwajibika mara moja na kuchukua hatua stahiki dhidi ya chombo husika, kwani athari ya uchochezi huo haiishii kwa Dk.Slaa na chama chake tu bali pia kitendo hicho kwa taathira yake ni hatari kwa taifa zima.

Kinachoshangaza na pengine kusikitisha zaidi ni suala hilo kuendelea kukuzwa na kulazimishwa kwa staili hiyo licha ya ukweli kuwa tayari Kanisa Katoliki lenyewe lilishakanusha rasmi madai ya kumtuma Dk. Slaa kugombea urais tangu ilipochapwa gazetini habari iliyotangulia, iliyokuwa na maudhui yanayofanana kidogo na habari hii iliyofuatia.

Uandishi wa aina hiyo unaonekana dhahiri kuwa na lengo la kuwapotosha na kuwagawa Watanzania wapige kura kidini pengine kwa matakwa na masilahi ya chama au mgombea wa urais anayeungwa mkono na chombo husika cha habari.

Hali hii inaweza kusababisha Watanzania wasio waangalifu kupumbazwa na habari hizo na kujikuta wakiacha kumchagua mgombea anayestahili na matokeo yake taifa kujikuta likipata viongozi wabovu waliochaguliwa kwa sababu ya dini au makabila yao badala ya sifa za uwezo wao wa kiuongozi. Kwa mantiki hiyo, nathubutu kusema tena hapa kwamba, habari ya namna hiyo hazina maslahi kwa taifa kwani kwa taathira yake zinaweza kuhujumu haki na utashi wa Watanzania kuchagua kiongozi atakayewafaa.

Aidha, nikumbushe kwamba si mara ya kwanza kwa gazeti hilo au mengineyo yenye muelekeo kama huo kuandika habari zenye kuhamsha hisia za ubaguzi kwa mtindo wa kuonyesha madai ya kuwepo ubaguzi. Katika kile kinachoonekana kuwa ni mkakati, mara zote hizo, CHADEMA ndiyo imekuwa mhanga mkuu wa habari hizo.

Mathalani, wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, waliandika kile walichokiita kuwa ni ukabila ndani ya CHADEMA, wakijaribu kuushawishi umma ukione kile kilichodaiwa kuwa ni upendeleo wa Wachaga (Uchaga) ndani ya chama hicho. Hilo likarudiwarudiwa mara kadhaa na kukuzwa zaidi hata baada ya uchaguzi ule.

Ilipokosa nguvu wakaandika madai kuwa CHADEMA ni chama cha watu wa Mkoa wa Kilimanjaro. Mkurugenzi wa Mambo ya Nchi za Nje wa chama hicho, John Mnyika, ambaye kabila lake ni Msukuma naye wakamchokonoa na kubaini kuwa mama yake ni Mpare na kutumia kabila hilo la mama yake kuhalalisha madai yao dhaifu kwamba CHADEMA ni chama cha watu wa Kilimanjaro. Vituko vitupu!

Madai ya chama cha Kilimanjaro yalipochuja yakaongezewa nguvu mpya, sasa chama hiki kikadaiwa kuwa ni chama cha upendeleo kwa watu wa ukanda wa kaskazini. Yote matatu, ‘Uchaga’, ‘Kilimanjaro’ na “Kanda ya kaskazini” yakarudiwarudiwa kwa miaka minne mfululizo yakishereheshwa na hoja dhaifu zilizoonekana kuupima au kuuchezea uwezo wa kufikiri wa Watanzania lakini wapi – propaganda hizo zilikosa mvuto. Madai yote yakakosa mashiko.

Chama kilichodaiwa cha Wachaga, cha Kilimanjaro, cha Kaskazini, juzi kilikuwa Musoma na Mwanza, jana kilikuwa Shinyanga na Kagera, kinafanya nini kote huko?

Mara zote uchambuzi makini ungeweza kujiridhisha pasipo shaka yoyote ile kuwa, habari hizo zilikuwa zikilenga tu kukiondolea imani chama hicho au viongozi wake ndani ya mioyo na fikra za Watanzania. Kinyume chake walengwa wa propaganda zote hizo (CHADEMA na uongozi wake) wameendelea kuimarika na kuonekana kuungwa mkono na Watanzania wa kada zote, wakiwemo wasio na dini, wenye dini na makabila yote. Sasa umeibuliwa wimbo mpya ‘udini na ukatoliki’, hii ndiyo santuri mpya nayo kama zilivyokuwa santuri zilizopita inaonekana kukosa mashabiki. Tusubiri tuone.

Kutoka Uchaga hadi Ukatoliki; tuwaeleweje watu hawa, tuvieleweje vyombo hivi vya habari, tuwaeleweje wanasiasa hawa? Jibu la msingi ni moja tu, nalo ni lile lililowahi kutolewa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, kwamba “wamefilisika kisiasa”.

Upande wanaoupigania umepwaya, hauna hoja za msingi za kujihalalisha kwa umma, ndiyo maana zinafanyika jitihada nyingine za pembeni zikijaribu kutumia ukabila na udini kuwatafutia uhalali mpya watawala walioshindwa kuthibitisha uhalali wao wakiwa madarakani.

Wanajua fika kwamba sekondari za kata si kigezo cha kumhalalisha mgombea wao mbele ya umma wa Watanzania waliojipatia elimu na maarifa kupitia shida za nchi yao licha ya kunyimwa elimu bora na serikali yao.

Wanajua fika kwamba vigogo wachache waliofikishwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa na matumizi mabaya ya madaraka sio kigezo cha msingi cha kumhalalisha mgombea wao aliyeshindwa kutumia vizuri madaraka yake kunusuru fedha na raslimali nyingi za umma.

Wanajua fika kwamba wasifu na uwezo wa mgombea wao hautoshi kumhalalisha mbele ya umma wa Watanzania utakapolinganishwa na wasifu na uwezo wa Dk.Slaa aliyevuta hisia za Watanzania wengi ndani ya wiki mbili tu tangu alipokubali kuwania wadhifa huu mkubwa.

Wana hofu ya msingi kuwa Dk. Slaa aliyefanya kazi kubwa jimboni, bungeni na nje ya Bunge kwa miaka kumi na tano sasa, amejipatia umaarufu, umashuhuri na uhalali mkubwa wa kupewa dhamana ya kuliongoza taifa kuliko yule aliyepewa dhamana hiyo lakini akalirudisha nyuma.

Wanajua fika kuwa hata jina la ‘Dokta’ linalotumiwa na mgombea wao ni la kupewa kwa heshima tu na wala halijatokana na kufikia ngazi ya elimu ya udaktari wa falsafa “PHD” aliyonayo Dk. Slaa. Kwa mantiki hiyo wanajua fika kuwa hawana miujiza hata ile ya kumtengenezea sifa za ziada mgombea wao na chama chao, sasa wamebakiwa na mkakati mmoja tu, nao ni kujaribu kuharibu sifa za Dk. Slaa kwa kuihusisha hatua yake ya kuwania urais na ukatoliki na historia yake ya kuwa padri, ili kuibua hisia za ubaguzi miongoni mwa Watanzania dhidi ya mwanasiasa huyo. Tukikubali kuingia kwenye mtego wa kutufanya anayetufaa tumuone hatufai, basi tutakuwa tumekubali kukwamisha harakati za kuufikia ukombozi mpya wa taifa letu. Tusikubali.

Wana falsafa wana msemo usemao: “Ni mjinga yule asiyesoma, lakini ni mjinga zaidi yule anayeamini kila kitu anachokisoma”. Tusome magazeti lakini tusiamini kila kitu tunachokisoma, yapo yanayokosewa kwa bahati mbaya na wakati mwingine yapo yanayoandikwa kwa makusudi kupotosha au kutimiza malengo fulani yasiyo na maslahi kwetu sisi kama wananchi.

Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuvichunguza na kuvifahamu vyombo vyote vya habari vinavyoandika na kuripoti habari za aina hiyo na hatimaye kuvipuuza na kuviacha vikijifia vyenyewe kwa ama kukosa soko au kukosa wasomaji kwa sababu ya habari hizo ambazo nathibitisha pasipo shaka yoyote ile kwamba hazilitendei haki wala kulitakia mema taifa hili.

Kwa aya hizi, nauenzi na kuueneza wasifu wa Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere, kwamba: “Hatutamkataa mtu kwa sababu ya kabila lake lakini hatutamchagua mtu kwa sababu ya kabila lake.” Vivyo hivyo, “haitatusaidia kumkataa mtu kwa sababu ya dini yake wala kumchagua mtu kwa sababu ya dini yake”. Tuweke mbele masilahi ya taifa letu.

No comments:

Post a Comment