Friday, December 2, 2011

Waraka wa Kinabo: Kuna umuhimu gani Wapinzani kuungana?

WATANZANIA wenzangu, kama nilivyosema katika waraka wangu kwenu wiki mbili zilizopita, ukombozi wa taifa letu dhidi ya umaskini, ujinga, maradhi na ufisadi, hauwezi kupatikana chini ya utawala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichoshindwa kufanya hivyo katika kipindi cha miaka 47 ya utawala wake.

Nilieleza kuwa CCM imeshathibitisha kupitia viongozi wake, makada, na utendaji wa serikali yake kuwa ni chama ambacho hakina dhamira ya dhati ya kusimamia uwajibikaji na adilifu kwa ajili ya maendeleo ya watu.

Maendeleo yaliyopatikana chini ya utawala wa chama hiki hayalingani na umri wa uhuru wetu wala utajiri wa rasilimali za nchi yetu. Aidha, hayalingani na wito wa wananchi katika kulipa kodi na kutoa michango ya kusaidia miradi ya maendeleo.

Mafanikio kidogo ambayo CCM imekuwa ikiyaita kuwa ni maendeleo na kuyatumia katika kila uchaguzi kulaghai wananchi, kwa kiasi kikubwa yanalingana na ufisadi uliokithiri nchini.

Wingi wa ufisadi ndio udogo wa maendeleo yetu! Katika kipindi hiki ambacho taifa letu linakabiliwa na matatizo makubwa ya kukithiri kwa ufisadi na kuongezeka kwa makali ya maisha, wajibu wetu mkuu unapaswa kuwa ni kutafakari njia mbadala ya kutufikisha kwenye ukombozi tunaouhitaji na kuifuata njia hiyo.

Mfumo wa siasa ya vyama vingi nchini ndiyo fursa ya kwanza tunayopaswa kuitumia. Uwepo wa vyama vya upinzani unatupa fursa ya kutafuta itikadi, sera, mipango na mikakati ya kutekeleza yale tunayoyahitaji. Tunahitaji kasi, ufanisi na uwajibikaji unaozidi ule ulioonyeshwa na CCM kwa kipindi cha miaka 47 sasa.

Hata hivyo, nguvu ya CCM siku zote imekuwa ikijenga hofu kwa jamii kuwa ni vigumu kwa chama chochote cha upinzani kuweza kuing’oa CCM madarakani.

Kwa sababu hii, imekuwa ikipendekezwa na kusisitizwa kwa muda mrefu kwamba, ili kuiondoa CCM madarakani, vyama vya upinzani nchini ni lazima vishirikiane na kusimamisha mgombea mmoja katika kiti cha urais, viti vya ubunge, udiwani na katika viti vya chaguzi za serikali za mitaa.

Leo waraka wangu kwenu unahusu mtazamo na imani hii kubwa iliyojengwa kwa wananchi, nawasihi tujiulize maswali haya: “Kuna umuhimu gani kwetu, wapinzani wakishirikiana ili kuing’oa CCM? Hivi ni kweli kuwa CCM haiwezi kung’olewa hadi vyama vya upinzani viungane au vishirikiane? Tutafakari pamoja.

Wahenga wetu waliowahi kuishi karne nyingi nyuma, walituusia kuwa umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Hata hivyo katika medani za siasa za sasa, nikizingatia uzoefu wa ushirikiano wa vyama vya siasa nchini na ule wa nchi jirani ya Kenya, nasita kukubaliana moja kwa moja na dhana ya vyama vya upinzani kuwa katika ubia wa kisiasa.

Muungano au ushirikiano wa vyama vya siasa ni jambo lenye mantiki lakini katika mfumo wa vyama vingi umoja wa vyama vya upinzani unaweza usiwe na tija kwa wananchi.

Ikiwa vyama vitakuwa kwenye ushirikiano au muungano wa kisiasa kwa lengo tu la kukitoa chama tawala madarakani, bila kujipanga jinsi watakavyoweza kuunda serikali na kuwaondolea wananchi umaskini na matatizo mengine yanayowakabili, muungano au ushirikiano huo unaweza kuwa ni wa madhara makubwa kwa taifa.

Hata kama CCM ni tatizo bado ushirikiano wowote wa vyama vya wapinzani wenye lengo tu la kuing’oa CCM madarakani hauwezi kuwa na manufaa kwa taifa. Kuiondoa CCM madarakani ni jambo moja na kuiletea Tanzania maendeleo ni jambo jingine.

Baadhi ya watu wamekuwa wazito kutofautisha mambo haya mawili ambayo yanapaswa kwenda pamoja. Lazima malengo yawe zaidi ya kuiondoa CCM madarakani, vinginevyo ushirikiano wa vyama vya upinzani dhidi ya chama kinachotawala hauwezi kuwa na mantiki wala manufaa kwa Watanzania.

Kwa mfano katika ushirikiano wa kisiasa unaoyumba au uliovunjika kati ya vyama vikuu vinne vya upinzani, Chadema, CUF, TLP na NCCRMageuzi, vyama hivi kila kimoja kina itikadi, sera na mtazamo tofauti kuhusu jinsi kitakavyoongoza nchi iwapo kitapata ridhaa hiyo kutoka kwa wananchi.

CUF inajitambulisha kama chama cha itikadi ya Kileberali, Chadema inafuata itikadi ya mrengo wa kati, na NCCR wana mguso wa kijamaa.

Ikiwa vyama hivi vitaendelea kushirikiana kwa lengo la kusimamisha mgombea mmoja ili kuitoa CCM madarakani, serikali itakayoundwa na vyama hivi itafuata sera zipi? Wenzetu wanaotaka vyama hivi vishirikiane au viungane wakiamini kuwa kwa kufanya hivyo CCM itang’olewa, hivi wameainisha uwiano wa sera na misimamo ya vyama hivi kabla ya kuvitaka viendelee kufanya hivyo? Binafsi, naamini kuwa tunapaswa kuamka zaidi na kuimarisha mazingira ya kidemokrasia badala ya kushikilia hoja ya vyama kuungana.

Sioni haja ya kuilazimisha jamii kuchagua rangi nyeusi na nyeupe tu, kama jamii tunapaswa kutambua kuwa kuna nyekundu, bluu na kahawia pia. Tuondoe dhana ya uwili, CCM na upinzani, ndiyo na hapana, ukweli na uongo! Dhana ya uwili ina tofauti ndogo sana na mfumo wa chama kimoja tuliokwisha kuuacha.

Kunatakiwa kuwepo ushindani wa fikra, hoja nzito na sera mbadala. Tusitengeneze NARC nyingine Tanzania, kama ile ya Kenya ambayo malengo yake yalikuwa kuiondoa KANU pekee.

Vyama viungane kama malengo, maono au itikadi zao zinawiana na si kwa lengo la kuing’oa CCM tu. Ushirikiano au muungano usio makini wa vyama vya upinzani vyenyewe, au chama tawala na vyama vya upinzani, unaweza kusababisha kuundwa kwa serikali kubwa sana pindi muungano huo unaposhinda uchaguzi.

Ukweli ni kwamba, sisi ni binadamu, hisia za uchama zitaendelea kuwepo hata baada ya chama kimoja kuundwa, watu wataangalia waliokuwa CUF wapewe majimbo mangapi kugombea, Chadema, TLP na kadhalika.

Iwapo muungano utashinda ipo hatari ya kuundwa serikali kubwa kwa minajili ya kuridhisha kila chama kilicho kwenye muungano au ushirikiano huo (iwapo sheria ya vyama vya siasa itarekebishwa.

Muungano unaweza kupata shinikizo la kuridhisha kila chama kilicho kwenye muungano husika kitoe viongozi wa kuunda serikali. Hapa ndipo tunapoweza kuwa na wizara moja yenye mawaziri zaidi ya watatu na matokeo yake ni kuwa na bajeti kubwa mno kwa ajili ya kugharamia shughuli za utawala serikalini kuliko miradi ya maendeleo kwa ajili ya wananchi.

Kwa hiyo ushirikiano wa vyama vya upinzani wenye lengo tu la kuing’oa CCM hauwezi kuwa na manufaa kwetu. Kwa sababu hii kuyumba au kuvunjika kwa ushirikiano wa Chadema, CUF, TLP na NCCRMageuzi hakuwezi kuwa na madhara yoyote ya msingi kwetu sisi wananchi.

Bila shaka kuyumba au kuvunjika kwa ushirikiano wa vyama hivi kutatupa fursa nzuri zaidi chama au vyama vyenye sera nzuri na dhamira ya dhati ya kuziba pengo la upungufu wa CCM.

Hivi ni kweli kuwa CCM haiwezi kung’olewa hadi vyama vya upinzani viungane au viwe katika ushirikiano wa kisiasa? Msingi wa swali hili ni kuwa wapo wanaoamini kuwa sababu kuu ya vyama vya upinzani kushindwa katika chaguzi zilizopita ni kutosimamisha mgombea mmoja.

Kwamba vimekuwa vikigawana kura na kuiacha CCM ikishinda. Kwamba ili vyama vya upinzani viweze kuishinda CCM ni lazima viungane au vishirikiane, vinginevyo CCM itatawala milele. Binafsi siamini hivyo, sikubaliani na ulazima huo.

Naamini kuwa chama kimoja cha siasa chenye dhamira ya kweli, sera nzuri na mikakati mizuri na endelevu ya kufanya siasa na inayoweza kuwaridhisha wananchi kuwa itawakomboa, kinaweza kuishinda CCM.

Chama chochote kinachoweza kuthibitisha uwezo na dhamira yake ya kuwatumikia wananchi kuanzia bungeni kinaweza kuaminiwa na umma na kupata ridhaa ya kuongoza dola chenyewe bila kulazimika kuungana na vyama vingine.

Uzoefu wa uchaguzi mkuu uliopita uliompa Rais Kikwete ushindi mkubwa wa zaidi ya asilimia 80 unaweza kuthibitisha imani yangu. Miongoni mwa vyama vilivyoshiriki kwenye uchaguzi ule katika kiti cha urais ni CCM, Chadema, CUF, TLP, NCCR-Mageuzi, PPT Maendeleo, Demokrasia Makini, DP na SAU.

Mgombea wa urais wa CCM katika uchaguzi ule, Jakaya Mrisho Kikwete alipata ushindi wa zaidi ya asilimia 80, maana yake ni kwamba tukichukua kura za vyama vya upinzani zaidi ya nane vilivyosimamisha wagombea wake bado zisingeweza kutosha kuzidi kura za mgombea wa CCM.

Vyama vyote vya upinzani vilivyoshiriki kwenye uchaguzi ule kiti cha urais vilipata si zaidi ya asilimia 19 ya kura, wakati Kikwete wa CCM alipata zaidi ya asilimia 80. Kwa manti hii hoja kwamba vyama vya upinzani hushindwa kwa sababu ya kugawana kura haina mashiko.

Hushindwa kwa sababu ya udhaifu wao na sababu nyingine zilizo nje ya udhaifu wao, likiwemo tatizo la mfumo wetu wa uchaguzi (tutajadili hili siku zijazo). Uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Tarime pia unaweza kuthibitisha mtazamo wangu, kwamba chama kimoja cha upinzani kikijijengea uaminifu kwa umma na kufanya siasa za makini, si tu kinaweza kuishinda CCM bali kinaweza kuvishinda vyama vingine vingi.

Katika uchaguzi wa Tarime, CCM, Chadema, NCCR-Mageuzi na DP kila kimoja kilisimamisha mgombea wake, lakini ni chama cha upinzani cha Chadema ndicho kilichoweza kuibuka na ushindi na kuvishinda vyama vingine vyote, ikiwemo CCM.

Nguvu ya Chadema na kampeni makini iliyofanywa na chama hiki kule Tarime inaweza kuenezwa nchi nzima na chama hiki kikaweza kuing’oa CCM madarakani na hatimaye kuongoza nchi kwa kufuata sera zake ikiwa wananchi wataridhia hivyo.

Aidha, nguvu ya Chama cha NCCR- Mageuzi iliyoonyeshwa nchi nzima katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, na nguvu ya CUF iliyoonyeshwa katika chaguzi zote tatu zilizopita, ule wa mwaka 1995, 2000 na mwaka 2005 kule kisiwani Zanzibar, zote zinathibitisha kuwa upo uwezekano mkubwa kwa CCM kung’olewa madarakani na chama kimoja cha upinzani iwapo kitajipanga na kuwa makini katika kufanya siasa zake.

Wajibu wetu kama wananchi ni kupima chama chenye muelekeo si tu wa kushinda katika uchaguzi lakini pia wa kutuongoza na kutufikisha kwenye ukombozi tunaouhitaji dhidi ya umaskini, ujinga, maradhi na umaskini.

Kuamini kuwa ili CCM ing’oke ni lazima wapinzani waungane ni kupotoka. Kutaka wapinzani waungane kwa lengo tu la kuing’oa CCM madarakani hakutatusaidia, ikiwa vyama vyenyewe vinapishana kisera na kiitikadi.

Tuendelee kutafakari na kuutafuta ukombozi wetu.

No comments:

Post a Comment