Tuesday, December 20, 2011

Katiba Mpya yayeyuka

Na Edward Kinabo

NDOTO ya Watanzania kupata katiba mpya imetoweka baada ya serikali ya rais Jakaya Kikwete kuamua kuunda tume ya kukusanya maoni ya katiba kabla ya kurekebisha sheria inayolalamikiwa, Tanzania Daima Jumatano limebaini.

Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani, amethibitisha wiki hii kwamba Serikali haina nia ya kuifanyia marekebisho Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 na kwamba kinachosubiriwa hivi sasa ni Mkuu huyo wa nchi kuunda tume ya mabadiliko ya katiba kwaajili ya kukusanya maoni.

Kombani akihojiwa kwenye mahafali ya Chuo cha Taaluma ya Habari jijini Dar es Salaam (DSJ), alisema sheria hiyo ni lazima tume hiyo iundwe kwanza kabla ya marekebisho yoyote kufanywa.

Msimamo huo unaonekana dhahiri kwenda kinyume na kile alichokubali Kikwete kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), walipokutana naye Ikulu jijini Dar es Salaam hivi karibuni, kwamba ipo haja ya sheria hiyo kufanyiwa marekebisho kabla ya kuanza kutumika.

Msimamo huo mpya unamaanisha kuwa tume hiyo itaundwa na wajumbe wa kuteuliwa na Rais chini ya utaratibu uliowekwa na sheria iliyosainiwa, jambo ambalo limekuwa likipingwa na wadau wengi.

Wanaopinga utaratibu huo wamekuwa wakisisitiza kuwa, “wajumbe wa tume wakiteuliwa na Rais hawatakuwa huru na watalazimika kulipa fadhila kwa Rais atakayewateua na chama chake (CCM)”

Wanasema utaratibu wa sheria hiyo ukitumika ni dhahiri kuwa tume itafanya kazi ya kuchakachua maoni muhimu ya wananchi na kuhakikisha inadumisha yote yanayotakiwa na CCM hata kama yatakuwa kinyume na matakwa ya wengi.

Wanatoa mfano kuwa wakati wananchi wengi wanaoonekana kukerwa na muungano wa serikali mbili na kutaka katiba mpya iruhusu muundo wa Serikali tatu, sera ya CCM siku zote imekuwa ni kudumisha serikali mbili.

Aidha, baadhi ya wadadisi wa masuala ya kisiasa wamelieleza Tanzania Daima Jumatano kuwa CCM haijawahi hata siku moja kuwa na ajenda ya kutaka katiba mpya.

Kwamba inachofanya sasa ni kujaribu tu kuwatuliza wananchi kwa kuwapa matumaini hewa kuwa katiba mpya inakuja, wakati wamepitisha sheria inayowawezesha kuutawala mchakato mzima na kuamua aina ya katiba waitakayo kwa maslahi yao ya kichama na kiserikali.

“CCM siku zote wamekuwa wakiipigania katiba ya sasa ibaki. Kama tutazubaa na kuacha sheria hii bila marekebisho, hakuna katiba mpya itakayotokea… maana tume itakuwa ni yao na vyombo vyote vya kuamua katiba kama bunge la katiba, mabaraza ya katiba na kura za maoni, vitatawaliwa nao”, ameeleza Jaji mmoja mstaafu kwa sharti la kutotajwa jina lake.

Chadema kupitia Waraka wao kwa Kikwete, walipendekeza badala ya wajumbe wa tume kuteuliwa na Rais pekee, sheria irekebishwe kuruhusu wajumbe kupatikana kwa kuchaguliwa kutoka kwenye taasisi za kiraia, kidini, kitaaluma, vyama vya siasa na wachache kuteuliwa na Rais, ili kuwa na tume huru na yenye uwakilishi mpana wa kulinda maslahi ya umma katika mchakato mzima wa katiba mpya.

Ili kuondoa uwezekano wa upande mmoja wa muungano kuingilia mambo yasiyo ya muungano na kuamua muelekeo wa kikatiba wa upande wa pili, chama hicho kikuu cha upinzani pia kilipendekeza kwa Rais kwamba kuundwe tume mbili za katiba, moja itakayokusanya na kuratibu maoni ya wananchi kuhusu katiba mpya kwa ajili ya masuala yasiyokuwa ya Muungano ya Tanganyika, na ya pili itakayokusanya na kuratibu maoni ya wananchi juu ya masuala ya Muungano.

Mbali na Chadema, makundi ya kijamii na asasi nyingi zimekuwa zikipinga tume ya katiba kuundwa na Rais na kutaka sheria nzima ifanyiwe marekebisho makubwa.

Baadhi ya makundi hayo ni pamoja na Chama cha Mawakili Tanganyika, Chama cha Majaji Wastaafu, Chama cha Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na asasi zaidi ya180 zinazounda Jukwaa la Katiba.

Wengine ni Umoja wa Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Umoja wa Madhehebu ya Kidini Tanzania (Inter-Religion Council for Peace in Tanzania (IRCPT) na watu mashuhuri kama Jaji Mkuu mstaafu, Barnabas Samatta na msomi mashuhuri nchini, Profesa Issa Shivji wamedaikatika mijadala inayoendelea nchi nzima

Mwisho.

No comments:

Post a Comment