Friday, December 2, 2011

Waraka wa Kinabo: Hawa wanachelewesha ukombozi wetu

WATANZANIA wenzangu, wazalendo wa kweli wa Tanzania yetu, tutaweza kuing’oa CCM? Leo waraka wangu unajaribu kufanya tafakuri ya swali hili kwenu. Binafsi nalitafakari, nikiwa na sababu kuu mbili zinazonisukuma kufanya hivyo.

Kwanza, kama nilivyowahi kuandika awali, kuing’oa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliyotawala nchi hii kwa zaidi ya miaka 47 (tangu TANU na ASP), ni muhimu mno katika kupisha mustakabali mpya wa ukombozi wa taifa letu dhidi ya umaskini, ujinga, maradhi na ufisadi. Katika hili nisisitize yafuatayo.

Ni muhimu CCM ing’oke kwani ndiyo chanzo na kikwazo kikuu cha matatizo yanayotukabili. Utawala wake wa muda mrefu, umekuwa wa kusuasua, wa kifisadi na usiokuwa na dhamira ya dhati ya kuwakomboa Watanzania.

Wingi wa raslimali na utajiri wa nchi yetu haviwiani na hali za maisha yetu, wala havilingani na umri wa uhuru wa nchi yetu, tangu tulipoupata mwaka 1961.

Kushindwa kwa CCM kumaliza au kupunguza umaskini wa nchi hii, kulibainishwa pia na hotuba ya bajeti mbadala ya kambi ya upinzani, iliyosomwa bungeni hivi karibuni na kiongozi wa kambi hiyo, Hamad Rashid Mohamed. Moja ya aya za hotuba hiyo, zilisema kama ifuatayo, ninanukuu:

‘‘Wakati CCM kinaendelea kupongezana kwa kunyosheana dole gumba, Watanzania wanaolala na njaa wameongezeka toka milioni 7.4 mwaka 1990 hadi kufikia milioni 14.4 mwaka 2007”, mwisho wa kunukuu.

Nikizingatia nukuu hiyo, ni muhimu CCM ing’oke ili tusitishe kasi hii ya ajabu ya kuongezeka kwa idadi ya maskini kila kukicha.

Ni muhimu CCM ing’oke kwani, kutokana na mfumo na kiwango cha kuchafuka kwake, hakuna tena uwezekano wa kutokea mtu atakayekuwa na uwezo wa kuleta mabadiliko kutoka ndani ya chama hicho.

Ni muhimu CCM ing’oke kwani wapo Watanzania wengi walio nje ya chama hicho, wenye uwezo wa kifikra na kiutendaji, wenye uchungu na nchi yao na wenye nia ya dhati ya kuikomboa nchi yao.

Pili, wakati ni muhimu kwa CCM kung’oka ili kupisha ukombozi mpya wa nchi hii, uzoefu wangu unaonyesha kuwa wapo watanzania wenzangu wenye mitazamo au imani zinazochangia sana kuchelewesha harakati za kuing’oa CCM kutoka madarakani.

Watanzania hao na mitazamo yao, naweza kuwagawanya katika makundi makuu matatu kama ifuatavyo;

Kundi la kwanza, ni lile la watu wasiojua, wasiojali au wasioamini kabisa kwamba siasa na uongozi wa serikali, vinaweza kufanikisha au kukwamisha jitihada za kutimiza ndoto za maisha yao.

Hili naliita kundi la kipekee. Naliita hivyo si kwa kulisifia bali ni kutokana na mtazamo wake wa kushtusha zaidi kulinganisha na makundi mengine nitakayoyajadili hapa chini. Kundi hili linaamini kuwa CCM ing’oke au ising’oke hilo si muhimu kwao.

Kwamba, itawale CCM, Cuf, CHADEMA, TLP, NCCR –Mageuzi au chama kingine chochote kile au kusiwe na serikali kabisa, wao hawajali, wanaona sawa tu.

Hawajali kwa sababu wanaona kufanikiwa, kukwama au kushindwa kwa maisha yao, hakuna uhusiano wowote na masuala ya kiserikali au utawala wa vyama vya siasa.

Hawa ndio wale ambao hawajiandikishi kupiga kura au wakijiandikisha hufanya hivyo kwa lengo la kupata vitambulisho tu lakini si kwa lengo la kutumia haki yao ya kuchagua chama au mgombea atakayeweza kuboresha maisha yao. Hawa pia ni wepesi sana kuuza shahada zao za kupigia kura pindi wanapofuatwa na viongozi au makada wa CCM.

Hawa wanaamini kuwa juhudi zao binafsi za kufanya biashara, kuchimba madini, sanaa, kuajiriwa, kulima na shughuli nyingine, zinatosha kabisa kutimiza ndoto za maisha yao.

Hawa hawapimi wala kujali athari chanya au hasi zitokanazo na maamuzi ya serikali. Baadhi yao wanapokwama kwenye shughuli za kutafuta mkate wao wa kila siku huamini wana nuksi, wamerogwa au Mungu hajapenda. Ni kawaida kuwasikia wenzetu hawa wakiizungumzia siasa kama ifuatavyo;

‘‘Jamani mie na hayo mambo ya siasa akaaa mwenzangu…siyawezi. Ashinde CCM, ashinde huyo CHADEMA, sijui na wale nani wengine wale, Cuf mie najionea yote sawa. Kwani huyo atakayeshinda ndiye atakayenipa ugali? Nikijiuzia vitumbua vyangu hapa nikapata unga wa kuwasongea ugali wanangu wakala, basi namshukuru Mungu. Hiyo siasa itanisaidia nini?

Hakika kundi hili lenye Watanzania wenye mtazamo huu, ndio kundi la kwanza na la msingi kabisa linalokwamisha au kuchelewesha kwa kiasi kikubwa harakati za ukombozi mpya wa nchi hii.

Kundi la pili, ni lile la watu wanaoamini kuwa CCM haistahili kung’oka na haitang’oka. Hawa wanaona CCM haistahili kung’oka kwa kuwa ni chama kizuri mno na kimeiongoza vema nchi hii katika kupata maendeleo na kudumisha amani, utulivu na umoja na mshikamano wa kitaifa. Kwa mantiki hiyo, wanaona kuwa ni halali CCM kuendelea kutawala.

Kwa watu hawa, hakuna chama chenye uwezo wa kuongoza nchi hii kama CCM kwani chama hicho ndicho kilichopigania uhuru wa nchi hii (tangu TANU na ASP). Hawa hupenda kusisitiza, ‘‘CCM ndiyo yenye uzoefu na nchi hii’’.

Wenzetu hawa wanaona CCM haiwezi kung’oka kwani licha ya kuiongoza vema nchi hii pia ni chama chenye nguvu mno, kinachokubalika kwa wanachi wengi. Hawaamini kama siku moja chama hiki kitang’oka. Wanaamini kitatawala milele na milele.

Hakika kundi hili la Watanzania wenye mtazamo huu nalo huchangia kwa kiasi kikubwa kuchelewesha ukombozi mpya wa taifa hili.

Kundi la tatu, ni lile la Watanzania wanaona kuwa CCM inastahili kung’oka kutoka serikalini, lakini hawaamini kuwa kama kuna chama au kutatokea chama kitakachokuwa na nguvu ya kuiong’oa CCM.

Kwa hawa, CCM inastahili kung’oka kwani hayo inayoyaita maendeleo ni kidogo mno kulinganisha na utajiri wa raslimali zilizopo katika nchi hii.

Wenzetu hawa hutumia werevu wao kulinganisha maendeleo yaliyofikiwa katika nchi nyingine zikiwemo zile tulizozitangulia kupata uhuru, mathalani Kenya, Botswana na Namibia na kugundua ni kwa kiasi gani CCM inavyowapotezea muda Watanzania.

Zaidi ya kutatizwa na ufukara uliokithiri, wenzetu hawa pia huona kuwa nchi yao imetawaliwa na matatizo mengi ya uonevu, unyonyaji, ubaguzi, upendeleo na ukandamizaji.

Kwa mantiki hiyo, shauku na sababu zao za kutaka CCM ing’oke zinafanana kabisa na sababu zile zile zilizowafanya mababu na mabibi zetu wapambane na wakoloni na hatimaye kufanikiwa kuwang’oa, wakiongozwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Hawa wanaona kuwa amani na utulivu, umoja na mshikamano wa taifa vinavyodaiwa kudumishwa na CCM ni muhimu lakini si kila kitu kwa ustawi wa maisha yao, ikiwa chama hicho kimeshindwa kuondoa au kupunguza umaskini, ujinga, maradhi na ufisadi, vinavyowatafuna wao na nchi yao.

Hawa huona kuwa nchi yetu imechelewa mno, na inaweza ikapata maendeleo ya haraka mno (ikapaa), ikiwa serikali ya CCM itang’oka kupisha serikali ya chama kingine mbadala (wasichokijua), kuleta maendeleo kama yaliyofikiwa katika nchi jirani.

Lakini tatizo la watu wa kundi hili kama nilivyosema hapo juu ni kwamba, hawaamini kama CCM itang’oka. Kimsingi, wanatamani CCM ing’oke tena haraka iwezekanavyo, lakini hawaamini kama itang’oka, kwa sababu zifuatazo:

Kwamba, CCM haitang’oka kwa sababu ni chama chenye nguvu mno, chenye pesa nyingi, kikiwa na mtandao mkubwa wa viongozi na makada, kuanzia ngazi za chini kabisa za mashina, matawi, mabalozi wa nyumba kumikumi, uongozi wa vijiji, vitongoji, mitaa, kata, jimbo, wilaya, mkoa hadi taifa, wakifanya kazi ya kuvuna wanachama na kudumisha utawala wa chama hicho.

Kwamba, CCM haitang’oka kwa sababu ni chama kinachoshikilia serikali tangu mwaka 1961 kikiwa na sauti kwa tume ya uchaguzi (NEC), mahakama, majeshi, idara ya usalama wa taifa, na vyombo vyote vya ulinzi na usalama ambavyo huweza kuvitumia vibaya kudumisha utawala wake hata wanapotokea kushindwa kwa kura. Kwamba CHADEMA, Cuf au TLP, vikishinda nani atawatangaza kuwa washindi?

Kwamba, CCM haitang’oka kwa sababu vyama vya upinzani ni dhaifu, havina nguvu. Havina mtandao wa kutosha kutoka ngazi za chini hadi juu. Havina pesa, havifiki vijijini kwenye watanzania wengi.

Tena wapo wanaodiriki kusema (wengine wasomi), kwamba vyama vyote vya upinzani havina sera, vimetawaliwa na migogoro tu na viongozi wake wana uchu wa madaraka, ubinafsi na ukabila.

Hakika, kundi hili nalo la Watanzania wenye mtazamo huu, huchangia kwa kiasi kikubwa kuchelewesha harakati za ukombozi wa taifa hili, ingawa linautamani ukombozi huo. Ni kundi lililokata tamaa, ni Watanzania wanaoona giza nene mbele ya safari ya ukombozi wa nchi hii.

Kimsingi makundi mawili ya mwisho, lile la pili na la tatu, yanaamini kuwa CCM haiwezi kung’oka, tofauti zao ni kwamba kundi la kwanza linaamini CCM haistahili kung’oka wakati hili la pili linaamini kuwa inastahili kung’oka lakini haitang’oka.

Mitizamo na imani za watanzania wa makundi yote hayo vinakwamisha au kuchelewesha ukombozi mpya wa nchi hii, kwa sababu kwa ujumla wake, watu wa makundi yote hayo wana sababu au hoja zinazowafanya wasijue, wapotoke au wasiwe sehemu ya harakati za ukombozi wanaopaswa kuupigania na kuupata.

Hata hivyo, hoja na mitazamo ya makundi yote hayo kama nilivyofafanua, si za kupuuza. Kwa kiasi kikubwa hoja hizo, iwe ni kwa usahihi au upotofu wake, ndizo zinazochangia kuifanya CCM ionekane kuwa na nguvu kubwa kupindukia.

Kwa tafsiri ya mitazamo, imani na hoja hizo za baadhi ya Watanzania wenzetu (unaweza kuwa ni mmoja wao), ni kwamba tupende tusipende, CCM itatawala karne nyingi mno, itatawala milele na milele, itatawala daima.

Je, ni kweli CCM itatawala daima kama wenzetu hao wanavyoamini, tena wakiwa na hoja zao nzito nzito kama hizo? Je, tutaweza kuing’oa CCM inayopaswa kung’oka ili kupisha mustakabali mpya wa ukombozi wa taifa letu?

‘‘Watanzania wenzangu, kupitia waraka wangu kwenu, kwa kujiamini kabisa, natangaza unabii wangu juu ya mustakabali mpya wa uongozi taifa letu, kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichotawala nchi hii kwa zaidi ya miaka 47 sasa, toka enzi za TANU na ASP, kitang’oka kutoka kwenye serikali ya nchi hii.

…Niwe hai au mfu, nina hakika unabii huu mtakatifu na unaopaswa kutokea kwa manufaa ya vizazi vya leo na kesho vya taifa hili, utatimia.

Ndiyo, unabii huu utatimia kupisha zama mpya za utawala wa nchi hii, utawala utakaoleta haki palipo na dhuluma, upendo palipo na chuki na kuchochea maendeleo ya haraka na ya usawa kwa watu wote, yatakayosimika umoja na mshikamano wa kweli wa Watanzania wote”.

Kimsingi, kutokana na mfumo wetu wa kisiasa na kisheria, CCM kama chama cha siasa kinapaswa kung’olewa na chama kingine cha siasa. Kwa mantiki hiyo, tunapozungumzia harakati za kuing’oa CCM kutoka madarakani tunazungumzia harakati za kisiasa zinazofanywa au zinazoweza kufanywa na chama fulani cha siasa katika kuuvuta na kuunganisha umma wa Watanzania, kuelewa hasara za kutawaliwa na CCM na kuchukua wajibu wa kukipigia kura nyingi chama husika cha upinzani, kiingie serikalini. Katika hili kuna mambo yafuatayo yakutiliwa maanan.

Kwanza, ili kuiong’oa CCM kwa lengo la kuepukana na utawala wake usiofaa ni lazima kuwapo au kuanzishwe chama mbadala, ambacho kwa dira yake, maadili, miiko yake na dhamira yake kitaweza kuunda serikali mbadala itakayoondoa au kupunguza kwa kiasi kikubwa ubovu wa CCM isiyotakiwa.

Pasipo kuzingatia hili, kunaweza kukatokea hatari ya kuing’oa CCM iliyopo madarakani na kukiingiza chama kingine madarakani kisicho na tofauti yoyote na CCM.

Pili, ikiwa chama hicho mbadala kipo, basi pamoja na uzuri wake wa kiitikadi, kisera na dhamira yake ya kiutendaji, ni lazima chama hicho kiweze kufanya harakati madhubuti za kisiasa ili ndio kiweze kuungwa mkono na kuingia madarakani.

Itikadi, sera, kujua matatizo ya wananchi na kuwa na dhamira nzuri ya kuwaongoza vema wananchi, havitoshi kukifanya chama husika kiingie madarakani. Ni lazima chama hicho kifanye siasa ya kuwafikia, kuwaelewesha na kuwashawishi wananchi kukiunga mkono.

Tatu, katika kufanya siasa hiyo, ni muhimu kwa chama kinachotaka kuwa mbadala wa CCM kifahamu mitazamo ya Watanzania walio wengi juu ya siasa za nchi na hasa serikali ya chama kilicho madarakani. Kama tulivyoona hapo juu, si Watanzania wote walio maskini wanataka CCM ing’oke. Kwa mfano katika kundi la kwanza tuliona kuna Watanzania wenzetu ambao wamepigika kama sisi, wakifanya shughuli za ubangaizaji, tena wakikumbana na vikwazo kadhaa vya kiutawala.

Lakini bado wenzetu hawa uelewa wao haujafikia hatua ya kuuona utawala (serikali) kama ndiyo kikwazo chao kikuu. Huamini kuwa hawana bahati (nuksi), wamerogwa, mambo tu hayajaenda vizuri, si riziki au Mungu hajapenda.

Kwa mfano huo, ni muhimu kwa chama kinachotaka kuing’oa CCM kuielewa mitazamo kama hii ya wananchi wenzetu, ili kiweze kubuni mikakati madhubuti ya kuwaelimisha wananchi jinsi matatizo yao yanavyosababishwa na serikali, na jinsi matatizo hayo yanavyoweza kuondolewa kwa kuking’oa chama kilichounda serikali hiyo na kukiweka kingine madarakani.

Nne, ni lazima chama husika kibuni mkakati madhubuti wa kuwafikia na kuzungumza au kuwasiliana vema na wananchi, ili wajue uzuri wa chama hicho, vinginevyo bila kufanyika siasa hiyo, wananchi hawatajua dhamira na dira nzuri ya chama hicho katika kuwakomboa.

Tano, ni lazima chama kinachotaka kuwa mbadala wa CCM kielewe vema mfumo usio wa haki wa kisiasa, kama moja ya kikwazo kikuu dhidi ya harakati zake za kisiasa. Suala hili ni muhimu kwani linabeba zile hoja nzito za mtazamo wa Watanzania wa kundi la tatu, kwamba ni vigumu kuing’oa CCM kutoka madarakani kwa sababu tume ya uchaguzi ni yao, majeshi yote ni yao (yapo chini yao), mahakama zao na serikali pamoja na vyombo vyake vyote kwa ujumla, ipo chini yao.

Katika hilo la tano, uzoefu unaonyesha kuwa kuna hoja kuu mbili zinazokidhana. Hoja ya kwanza ni ile inayosema kuwa hakuna chama cha upinzani - hata kiwe kizuri vipi, kitakachoweza kuing’oa CCM hadi kwanza mfumo wa kisiasa utakaporekebishwa ili kujenga uwanja sawa wa ushindani kisiasa kwa vyama vyote.

Hoja ya pili inasema hivi, kwa kuwa chama kilicho madarakani (CCM), ndicho kilichouweka huo mfumo mbaya wa kisiasa ili kipendelewe na mfumo huo na kudumisha utawala wake, basi ni vigumu kwa chama hicho (kinachoshikilia makali), kukubali kuurekebisha mfumo huo, kwani kinajua fika kikifanya hivyo kitakuwa kinahatarisha nafasi yake ya kuwa madarakani.

Hoja hii inahitimisha kwa kusema hivi, njia muafaka lakini iliyo ngumu ni ile ya chama hicho mbadala kuamua kushindana na CCM ikitumia mfumo huu huu mbaya wa kisiasa kwani hakuna uwezekano wa CCM hiyo kukubali kuurekebisha.

Hoja hii ya pili pia inapinga mtazamo mwingine mwepesi unaovitaka vyama vya upinzani visusie uchaguzi hadi serikali ya CCM itakapokubali kurekebisha mfumo wa kisiasa kwa kuunda tume huru ya uchaguzi na kurekebisha sheria kadhaa za uchaguzi zinazokibeba chama hicho. Inahitimisha ikisema kuwa kususia chaguzi hakutaizuia CCM kuendelea kutawala, huku ikihalalisha utawala wake kauli mbalimbali za propaganda kama;

‘‘Wapinzani wameshindwa siasa, wamekubali tutawale baada ya kuona hawakubaliki”

Binafsi naungana na hoja hii ya pili, kwamba ni vigumu kwa serikali ya CCM kukubali kurekebisha mfumo wa kisiasa kwani uhai wa chama hicho unabebwa kwa kiasi kikubwa na mfumo huo. Kwa maneno mengine, tume huru ya uchaguzi itajenga uwezekano wa dhahiri wa chama hicho kushindwa uchaguzi kama hakitakubalika, kama vinavyoshindwa vyama vingine.

Uzoefu mdogo wa matukio ya kisiasa yaliyojiri nchi kwetu tangu kuanza kwa mfumo wa siasa za vyama vingi, unaashiria kuwa upo uwezekano wa CCM kung’olewa chini ya mfumo huu huu wa siasa tulionao. Nitoe mifano ifuatayo:

Chama cha Wananchi (CUF), karibu katika chaguzi zote, kimeweza kushinda viti vyote vya ubunge na uwakilishi kule kisiwani Pemba. Cuf imekuwa ikishinda katika mfumo huu huu wa kisiasa unaoibeba sana CCM, na si kweli kwamba CCM imekuwa ikiwaachia Cuf kushinda kisiwa chote cha Pemba. Wamekuwa wakikitamani sana lakini huzidiwa na kushindwa.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), nacho kimeweza kushinda viti vingi sana vya udiwani katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2005. CHADEMA hivi sasa ina madiwani takribani 102 nchi nzima. Hawa walipatikana wakati tume yetu sio huru na wala haitendi haki vya kutosha.

Aidha, chama hiki kiliweza pia kushinda chaguzi za ubunge mwaka 2005, kule Tarime, Mpanda Kati, Kigoma Kaskazini, Moshi Mjini na Karatu. Kutokana na ushindi wake huo, CHADEMA kikapata nafasi ya kuongoza serikali za halmashauri ya Karatu, Tarime na Kigoma ujiji. Hapa pia ni vema ikazingitiwa kuwa ushindi wote huu na mafanikio yote haya, yalipatikana katika uchaguzi ambao ulisimamiwa na tume isiyo huru tena ikisimamia sheria kadhaa za uchaguzi zinazoipa CCM mwanya wa kujifanya washindi. Huko kote, CCM walijaribu kufanya mbinu za kuungwa mkono walishindwa, walijaribu pia kufanya hia za kupoka ushindi nazo zilishindwa.

Kutokana na mifano hiyo, tunapata funzo kuwa Watanzania tunaweza kabisa kuishinda na kuing’oa CCM hata kama majeshi ni yao, tume ya uchaguzi yao, na mahakama ziko chini ya serikali ya chama hicho. Msingi wa uwezo wetu huo unajikita katika falsafa ya nguvu umma kuwa kubwa zaidi kuliko nguvu ya utawala (serikali) na vyombo vyake.

Hii inatuashiria kuwa iwapo umma wa Watanzania wa maeneo yote utaelimishwa kisiasa juu ya ubaya wa CCM na kuhamasishwa kuchukua wajibu wa kuing’oa bila uwoga kama ilivyofanyika kule Pemba, Tarime, Karatu, Moshi Mjini, Mpanda Kati, Kigoma Kaskazini na Kigoma Ujiji, basi Tanzania yetu itaweza kabisa kujikomboa kutoka kwenye utawala dhalimu wa CCM.

Tunaweza kupata rais na wabunge wengi kutoka chama mbadala cha upinzani, ikiwa tu umma wote utaelemishwa vema, kuhamsishwa na kutiwa ujasiri wa kutosha kama ilivyofanyika katika maeneo hayo niliyoyatolea mfano.

Nguvu ya umma wenye ujasiri wa kutosha inaweza kabisa kuwafanya vijana wetu walio kwenye majeshi kutothubutu kuipendelea CCM. Vijana walio kwenye vyombo vya ulinzi na usalama vinavyoibeba CCM leo hii, wanaweza kabisa kuchotwa na mwamko wa nguvu ya umma wa Watanzania walio wengi na kujikuta wakiiasi CCM na kutenda haki, ili kuepuka kumwaga damu za Watanzania wenzao. Hali kama hiyo au inayofanana na hiyo ndiyo iliyotokea katika maeneo kadhaa ambayo vyama vya upinzani vimeweza kushinda.

Kumbe inawezekana kabisa kwa CCM kung’olewa kutoka madarakani katika mazingira haya haya tuliyonayo!. Kinachotakiwa ni uwepo wa chama mbadala kinachoweza kuwaelimisha, kuwaunganisha, kuwahamasisha na kuwatia ujasiri Watanzania walio wengi katika kuikataa na kuing’oa CCM.

No comments:

Post a Comment