Thursday, December 22, 2011

Waraka wa Msigwa kwa viongozi wa dini Tanzania: Kuweni macho na wanasiasa hawa...

Kwa nafasi yangu kama raia, Mbunge ninayewakilisha wananchi wa Jimbo la Iringa Mjini na Watanzania wote kwa ujumla na mmoja wa viongozi wa dini/dhehebu nchini, naomba kutumia fursa yenu na ya vyombo vyenu vya habari kutoa ujumbe mahsusi kwa viongozi wenzangu wa kidini kwa manufaa ya taifa letu.

Ninapowasilisha salaam zangu hizi za X-Mas na Mwaka mpya wa 2012, ningependa kusisitiza yafuatayo kwa viongozi wenzangu wa dini, kuhusiana na nini hasa unapaswa kuwa wajibu wetu kuhusiana na mwenendo wa viongozi wetu wa kisiasa (mimi pia nikiwa mmoja wao);

1. Nianze kwa, kuwapongeza viongozi wenzangu wote wa dini waliojitokeza hadharani au kupitia vyombo vya habari hivi karibuni kupinga kusudio au mpango wa kuongeza posho za vikao kwa wabunge. Suala hili limegusa hisia za Watanzania wengi wakiwemo viongozi wenzangu wa dini ambao nami naungana nao kuzipinga nikisisitiza msimamo wa siku nyingi wa chama chetu (Chadema).

2. Pongezi hizi zinazingatia ukweli kuwa katika suala hili la posho,Baadhi ya viongozi wa dini wameweza kuchukua wajibu wao kikamilifu wa kuwa juu ya wanasiasa wenye malengo mabaya tofauti na desturi iliyoanza kujengeka hivi karibuni ya baadhi ya wanasiasa hususan wale wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kupenda kuwatumia vibaya baadhi ya viongozi wa dini na nyumba za ibada kama sabuni ya kujisafishia uchafu wao na ngazi ya kufikia malengo ya kuutafuta urais au ubunge na udiwani (uongozi mchafu). Ingawa kanisa ni mahali pa kusafishwa uchafu na kila mtu anakaribishwa, lakini tumkumbuke yule Simon Mchawi katika kitabu cha matendo ya mitume,aliyejaribu kununua kipawa cha Roho mtakatifu kwa faida yake binafsi, ndipo mtumishi wa Mungu Petro alipomwambia apotelee mbali pamoja na pesa yake.

3. Nawasihi viongozi wa dini wenzangu kwamba kamwe tusikubali kuwa mawakala wa kufanikisha mbio za urais mchafu. Tusikubali kuwa chini ya wanasiasa maana jukumu letu la kuwanusuru wanadamu kiroho kwa kuwaongoza kumcha Mungu, ni jukumu zito na kubwa kuliko uroho wa madaraka unaowakimbiza baadhi ya wanasiasa kwenye nyumba za ibada.

4. Ni udhalilishaji mkubwa wa huduma ya kiroho pale viongozi wa dini tunapowakaribisha wanasiasa kufanya shughuli kama za uzinduzi wa makanisa au albamu za nyimbo za kidini kana kwamba wao ndio wenye upako, utukufu na mamlaka zaidi ya kubariki kinachozinduliwa kuliko sisi viongozi wa dini wenyewe.

5. Tabia kama hii ya kuwatanguliza mbele wanasiasa kwenye shughuli za kiroho badala ya kuacha huduma hii ijitegemee yenyewe (maana Mungu ni Mkuu na mwenye uwezo kuliko siasa), kwa namna moja au nyingine imekuwa ndio kichocheo cha kufanya wanasiasa kutafuta pesa kwa gharama yoyote, ilimradi wakiitwa kwenye mialiko hiyo waweze kutoa fungu kubwa wakiamini itawajenga kisiasa hata kama hawana nia ya kweli na Mungu.

6. Tusikubali kamwe kutumiwa vibaya na wanasiasa wanaojipenyeza kwenye matukio mbalimbali kama ya harambee na uzinduzi wa albamu za nyimbo za kiinjili, kwa lengo la kujitangaza, kujisafisha na kujipendekeza kwa umma uliowakataa au kukosa imani nao.

7. Tusikubali nyumba takatifu za ibada zigeuzwe viwanja vya kampeni za kisiasa na wala tusiwe chanzo cha kuiingiza nchi yetu katika mgawanyiko na machafuko ya kidini kwasababu tu ya kuwabeba baadhi ya wanasiasa ambao ama kwa sababu ya uchafu wao au umma kukosa imani nao, wameona hawawezi tena kuwa na uhalali wa kujitangaza wala kujijenga tena kwenye majukwaa ya kisiasa bila kwanza kukimbilia makanisani. Binafsi naamini, mwanasiasa msafi anayejiamini na anayemcha Mungu kwelikweli haitaji harambee au tukio lolote la kujinadi kanisani , maana huko si pahali pake.

8. Najua kuwa Watanzania wengi wanakerwa na tabia ya baadhi ya sisi viongozi wa dini kama maaskofu, wachungaji na mapadri kubabaikia wanasiasa kwa kiasi cha kuonekana wanaidhalilisha huduma hii kuu. Kanisa likitakiwa kuzinduliwa – mwanasiasa, uzinduzi wa nyimbo ya injili – mwanasiasa, ununuzi wa magitaa – mwanasiasa, ununuzi wa maspika – mwanasiasa. Hivi hawa wanasiasa wana upako gani kana kwamba kazi ya Mungu haiwezi kufanyika bila wao?

9. Tunapokwenda kusherehekea siku kuu hii ya X Mas na Mwaka Mpya, ninawasihi tena viongozi wenzangu wa kidini, kwamba tumkumbuke nabii Baalam ambaye vitabu vitakatifu vinaeleza jinsi alivyoifanyia biashara huduma yake ya kinabii mpaka alisababisha Punda aongee;

Tumkumbuke mtumishi wa nabii Elisha, aliyeitwa Gehazi, ambaye vitabu vitakatifu vinatufundisha kwamba alipenda pesa na zawadi akasahau mwito wake wa kitume mpaka ukoma wa Nahaman ukahamia mwilini mwake;

Tumkumbuke Esau aliyeuza haki ya uzaliwa wake wa kwanza kwa njaa ya muda mfupi (dengu,mlo moja tu);

Na tumkumbuke Yuda Eskarioti ambaye alimuuza mwokozi wetu, Yesu Kiristu, kwa vipande thelathini vya fedha, na kwa hiyo, sisi viongozi wa dini tusikubali kamwe kuwauza Watanzania wenzetu kwa pesa za wanasiasa wachafu.

10. Nasisitiza tena, kwamba sisi viongozi wa dini tunapaswa kuwa viongozi na sio wafuasi wa wanasiasa, tunapaswa kuwaonyesha njia wanadamu wote wakiwemo wanasiasa na sio wanasiasa watuonyeshe njia sisi, maana kufanya hivyo ni kulishusha thamani neno la Mungu.

11. Naamini kama taifa kwa ujumla tuna hali za duni za kimaisha zinazotugusa pia sisi viongozi wa kiroho, lakini hii isisababishe tukasahau misingi yetu ya kitume kana kwamba Mungu aliyetuita ametuacha. Naamini sisi viongozi wa dini tukisimama imara bila kuyumba, Tanzania yetu inayougua umaskini, ujinga, maradhi na ufisadi, hatimaye itaponywa. Hizi ndio salamu zangu za mwaka mpya kwa viongozi wa dini ambao naamini kupitia wao Watanzania wote wataongozwa vema

Nawatakia kheri na fanaka ya X- Mas na Mwaka Mpya.
Mungu ibariki Tanzania.

Mchungaji Peter Msigwa
Mbunge Jimbo la Iringa Mjini

No comments:

Post a Comment